Ilikuwa mwishoni wa mwaka 2008, nilimuona mtu mmoja akitumia iPhone 3GS, wakati huo ikionekana kama iPhone 6/6 Plus zilivyo sasa. Nilitumia dakika kadhaa katika kuiangalia simu ile lakini kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kusogea nilijiuliza baadhi ya maswali kichwani, "ni kweli hii ndiyo iPhone watu wanayoongelea?"," au pengine hii ni bandia?".... na mengine mengi!
Nadhani maswali hayo yaliyotokana na mimi kuwa na mategemeo makubwa sana kuliko uhalisia wa iPhone 3GS(over anticipation). Vile nilivyosikia watu wanavyoiongelea nilitengeneza picha kubwa sana akilini. Wakati huo, nilikuwa mpenzi mkubwa wa smartphones za Nokia zilizokuwa zinatumia Symbian OS(haipo tena). Symbian OS, iliyokuwa ikitumika katika smartphones za Nokia ilikuwa maarufu sana miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2008, ni Android OS ya enzi hizo unaweza kusema! Pengine sikuvutiwa na iPhone ile kwa sababu nilitegemea itakuwa kama smartphone ya Nokia lakini iliyo bora zaidi(more advanced).
Mwaka 2009, mnamo mwezi Juni. Niliona smartphone ya BlackBerry kwa mara ya kwanza katika maisha yangu. Tangu nikiwa mdogo nimekuwa nikipendelea sana vifaa vya kielectroniki hasa simu na saa. Sijawahi kupata furaha ya moyo kama niliyowahi pata siku ile(Eureka moment), ni kama vile mtu yule alinipa simu ile kama zawadi. Nilipatwa na mshangao wa hali ya juu sana, na nikasema hii ndiyo simu inayotoa maana halisi ya smartphone. Kwa muda ule simu hizi zilikuwa gharama sana, ilikuwa ni ngumu kumiliki simu hii kama hutahitaji kutumia pesa nyingi katika manunuzi ya simu, miaka hii simu za kawaida(feature phones) ndizo zilikuwa zikitumika sana.