Jun 26, 2015

BlackBerry inayotumia Android OS! wazo zuri?

Ni takribani wiki mbili sasa zimekuwepo tetesi nyingi mtandaoni zihusuzo kampuni ya BlackBerry kuwa na mipango ya kutengeneza smartphone ambayo itatumia operating system(OS) inayomilikiwa na Google, Android OS. Wakanada hawa kwa sasa wapo katika mahangaiko ya kurudisha soko la smartphones zao ambalo lilipokonywa na kampuni kama Apple na Samsung miaka takribani sita iliyopita. Tangu kuwepo kwa uongozi wa Bwana John Chen ambaye ni mkurugenzi(CEO) wa kampuni hii kwa sasa, BlackBerry imekuwa ikiona mafanikio japokuwa ni taratibu katika nyanja mbalimbali za biashara zao.

John Chen

Kampuni hii haifanyi tu biashara ya kutengeneza smartphones, inajihusisha na biashara ya kutengeneza programu(softwares) kama QNX ambayo inatumika hasa katika kusaidia ufanyaji kazi wa mifumo ya magari, mitambo ya viwanda, mitambo mikubwa ya upasuaji katika mahospitali na hata katika smartphones za BlackBerry. Kampuni nyingi za magari  kama Ford Motor, Volvo, Mercedes Benz, Porsche, BMW, Audi na  Maserati zinatumia mfumo wa QNX katika modeli nyingi za magari yao.
Makampuni makubwa na maarufu ya mambo ya umeme kama Siemens AG na General Electric(GE) wanatumia software ya QNX kwa kiwango kikubwa. Watumiaji wote niliowataja na wengine ambayo sijawataja wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta faida kwa kampuni ya BlackBerry. Na ndiyo maana pamoja na hasara aliyoipata mwaka 2013, takribani dola za kimarekani bilioni 4.4( takribani trilioni tisa za kitanzania), lakini bado aliendelea kuwepo kwa sababu ya biashara ya software, hasa QNX.

Touchscreen display iliyopo katika dashboard ya Mercedes Benz CLA45 AMG inakupa uwezo wa kutumia QNX software katika kufanya settings za automations za gari hili.

Si QNX tu, BlackBerry pia anatoa huduma ya mawasiliano na ufanyaji kazi kwa usalama zaidi katika makampuni na taasisi mbalimbali duniani, ziwe ni za binafsi au za serikali na hata zile za siri na nyeti(sensitive), mfano NSA(National Security Agency)! huduma hii inafahamika kama BlackBerry Enterprise Server(BES). Pamoja na kuwepo kwa Android na Apple, bado makampuni mengi makubwa duniani kama Exxon Mobil na mengineyo wanatumia smartphones za BlackBerry kwa ajili ya ufanyaji wao wa kazi, kesi ndogo ya kuonyesha matumizi ya BlackBerry ni wakati kampuni ya Sony Pictures ilipodukuliwa (hacked) mwishoni mwa mwaka jana na servers zake zote kutolewa mtandaoni (offline), katika muda huu wafanyakazi wa kampuni hii walitumia smartphones za BlackBerry katika kuendelea kufanya mawasiliano kwa usalama zaidi.

Mafanikio ya BlackBerry hayapo katika smartphones kwa sasa. Lakini hii haiwafanyi kukata tamaa kabisa katika nyanja hii. Baada ya kuingia kwa Bwana John Chen mengi mazuri yametokea na hata BlackBerry imeona mwinuko katika mapato yake. Aliwahi kusema "Nitaendelea na biashara ya smartphones kama tu itaonyesha kuleta faida, kama haitakuwa na faida sitajiuliza mara mbili kuachana nayo".   Jumanne iliyopita katika mahojiano ya televisheni ya CNBC alisema" Tunangeneza smartphones zilizo na usalama wa hali ya juu, na BlackBerry ndiyo smartphone iliyo na usalama kuliko zote. Kwa hivyo, kama ninaweza kupata namna ya kufanya smartphone ya Android kuwa na usalama wa hali ya juu, nitaitengeneza pia". Alisema haya kutokana na tetesi za BlackBerry kutaka kutengeneza smartphone itayotumia Android OS. Kauli yake ya hivi karibuni inaonyesha wazi anaanza kuona mafanikio katika biashara ya smartphones za BlackBerry 10 OS.

Kila kampuni sasa hivi inatamani kuwa na usalama kama alionao BlackBerry. Samsung, kwa muda sasa anajitahidi sana kufanya simu zake si kuwa tu za matumizi kwa watu wa kawaida bali hata kwa makampuni makubwa na taasisi mbalimbali zilizo za siri na nyeti(sensitive).

Mwaka 2013, Samsung Galaxy S4 ilipitishwa(approved) kutumika rasmi na wafanyakazi na viongozi wa  Pentagon(makao makuu ya idara ya usalama nchini Marekani). Si Galaxy S4 kama yako! hii ni maalumu kwa ajili ya sehemu za usalama(Limited Edition). Na modeli zao zilizofuatia kama Galaxy S5 na za sasa Galaxy S6 na S6 Edge zinaendelea kutumika. Samsung Knox ambayo inafanana na BlackBerry Enterprise Server(BES) inaanza kupata umaarufu taratibu na hivi karibuni Samsung ameingia ubia na BlackBerry katika kupata msaada wa kuifanya Knox kuwa salama zaidi na zaidi.  Haya yote ni katika harakati za Samsung kutaka kuwa kama BlackBerry katika suala la usalama.

Samsung wameweka neno "enterprise" katika moja ya tangazo la Galaxy S6 ili kukujuza kwamba wao ni mbadala wa BlackBerry!

Huwezi kujua, pengine ujio wa smartphone ya BlackBerry inayotumia Android OS utaleta zama (era) mpya za mapinduzi ya smartphones kama ilivyokuwa mwaka 2007 kwa iPhone. Tetesi zinadai kwamba smartphone hii itapewa jina la "Venice", ikiwa na processor yenye CPU sita( Hexacore) katika mfumo wa 64 bit na katika speed ya 1.8GHz, itakuwa na RAM ya 3GB na pia itatumia chipset ya kampuni ya Qualcomm ya Snapdragon 808 SoC(System on Chip). Camera ya nyuma ikiwa na 18MP na ya mbele ikiwa na 5MP.

Hii ni hatua nzuri sana waliyoamua kuifikia na italeta chachu kubwa ya mabadiliko katika soko la smartphones. Smartphones za BlackBerry 10 OS kwa sasa zinakubali kutumia apps za Android lakini nadhani watu wanahitaji uzoefu(experience) kamili wa Android OS katika smartphone ya BlackBerry! 

No comments :

Post a Comment