Jul 14, 2015

Teknolojia inabadili asili yetu.

Teknolojia inazidi kukua siku hadi siku, na kwa kasi ya ajabu sana. Kama wanadamu, tunatakiwa tambua ya kwamba " unapotumia sana mawasiliano ya internet na ndivyo unajitenga na mawasiliano ya kidunia(physical interactions)". Teknolojia inatuondoa katika mazingira yanayotuzunguka na kutupeleka katika mazingira ambayo si halisi, tuna marafiki wengi wa mitandaoni kuliko marafiki tulionao shule au kazini. Tunatumia muda mwingi katika smartphones zetu kuliko kuongea na wale wanaotuzunguka.

Miaka ya zamani, kabla ya teknolojia kuitawala dunia watu walikuwa wakienda sehemu wasizozijua kwa kuelekezwa na mtu mwingine au kutumia ramani iliyopo katika karatasi. Tofauti na siku hizi, hatujui hata kusoma ramani, tunapata shida kujua alama za barabarani na hatuna muda wa kusoma maelezo yaliyopo njiani na katika majengo. Unaenda sehemu usiyofahamu? Sawa! Google Maps itakuelekeza kuanzia ulipo na upite wapi mpaka kufika unapohitaji kwenda, rahisi sana eeh!


Smartphones na wearable devices kama smartwatches na fitness trackers zina uwezo wa kutuambia tumetembea hatua ngapi kwa siku, tumepunguza uzito kiasi gani na mambo mengine mengi mno. Jokofu(fridge) linaweza tuma taarifa katika smartphone yako kukujulisha ni mahitaji yapi yanakaribia kuisha ndani yake, huna haja tena ya kulifungua na kukagua na kupoteza muda. Haya yote ni faida kubwa sana kwetu kwa sababu huokoa muda na kufanya maisha kuwa rahisi mno.
Fridge ya Samsung itumiayo Android OS.

Ingawa tuna apps lukuki katika smartphone zetu zinazotuelekeza jinsi ya kula mlo wenye kuleta afya, njia bora za kufanya mazoezi na kujipa mapumziko, jinsi ya kupika chakula bora, namna ya kupangilia muda kwa ufanisi zaidi, jinsi ya kuendesha gari kwa umakini na kufata alama za barabarani na mengine mengi. Lakini afya zetu si nzuri ukilinganisha na watu wa zamani, hatujui namna ya kupangilia muda wetu, ni madereva wabaya na wenye vurugu mno, maisha yetu yana msongo wa mawazo kila kukicha, tofauti kabisa na watu wa miaka ya zamani.

Teknolojia imefanya mengi mno katika kumletea mwanadamu maendeleo, ukiangalia maisha ya watu wengi yanaokolewa mahospitalini kutokana ma matumizi ya vifaa vilivyo na teknolojia ya hali ya juu, si shida tena kufanya mawasiliano kokote duniani, uzalishaji umezidi kuongezeka na faida nyingine nyingi nyingi. Lakini, teknolojia hii inatufanya kupoteza maarifa ya kujua kufanya vitu vingi vya msingi(basic things). Kwa nini ufue kwa mkono? Mashine iko pale! huhitaji kujua muelekeo wa unapokwenda, GPS navigator ipo katika gari yako kwa ajili ya kazi hiyo. Changamoto ni kubwa sana katika teknolojia!

No comments :

Post a Comment