Nov 8, 2014

Upofu tulionao katika teknolojia.

"Teknolojia", neno ambalo linaendesha maisha yetu ya kila siku kwa kiasi kikubwa sana. Katika hii dunia, kuna makundi mbalimbali ya watu ukiwatofautisha katika nyanja ya teknolojia. Wale ambao wana uelewa mkubwa sana wa teknolojia, wale wenye uelewa wa kawaida katika teknolojia, wale wasio na uelewa kabisa kuhusu teknolojia na wale wasiotaka kabisa kujua kuhusu teknolojia. Pamoja na kwamba tunaweza fahamu vitu vingi vinavyohusiana na teknolojia na manufaa yake kwa ujumla, wakati mwingine hali hii inatufanya kuwa wapofu katika upande mwingine wa teknolojia tuliyonayo.



Watu wengi huamini ya kwamba bidhaa mpya za kiteknolojia zinapokuja kwa watumiaji huwa zinakabiliana na wakati mgumu sana kuweza kutambulika na pia kuwafanya watu kuona manufaa yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo. Nitakupa mfano mmoja ambao umekuwepo kwa muda mrefu, na ni maarufu pia. Mwaka 1977, marehemu Ken Olsen alisema "hakuna sababu ya maana kuweza kufanya watu kuhitaji kutumia kompyuta majumbani mwao", alisema kauli hii muda ambapo kompyuta za binafsi(personal computers) zilikuwa zinaingia sokoni. Unaweza dhani ya kwamba mtu huyu alikuwa ni mwenye uelewa mdogo wa teknolojia kwa kusema kauli hii, hasa katika mambo ya kompyuta, la hasha. Mtu huyu alikuwa ni mmiliki wa kampuni ya Digital Equipment Corporation(DEC)! kampuni hii ilikuwa ikijishughulisha na utengenezaji wa kompyuta hasa zilizokuwa zikitumika katika maofisi makubwa, viwanda na kadhalika, na pia ni mmoja wa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika teknolojia ya kompyuta na mambo ya unajimu(cosmonautics).


Kuna wakati mwingine, kuwa karibu sana na teknolojia, kuifahamu kwa undani, kufanya majaribio na tafiti mbalimbali kunakufanya uwe mpofu katika upande mwingine wa teknolojia hiyohiyo. Alikuwa akiwaza ni vipi ataweza kuboresha kompyuta zitumikazo viwandani na sehemu kubwa za uzalishaji, kwa upande wa pili hakuwahi pata wazo kwamba inawezekana kuhitaji kompyuta katika shughuli ndogondogo ambazo zinaweza kufanyika majumbani. Hali hii inatokea kwa sababu unapofanya tafiti ili kutengeneza bidhaa ya kiteknolojia huwa unakuwa na malengo fulani, lakini malengo haya yanakufumba macho katika matumizi mengine ya bidhaa hiyo. Unaweza waza kutengeneza kipaza sauti(microphone) kwa mfano, lakini wazo la kutengeneza kifaa kitachoweza kurekodi sauti inayochukuliwa na microphone hiyo lisikujie kichwani hata kidogo na baada ya muda kupita katika uvumbuzi wako anakuja mtu anafanyia marekebisho kidogo tu ya kuongeza kifaa cha kurekodi sauti. Hapo umekuwa na upofu wa kiteknolojia, ni ngumu wengi wetu kukubali kwamba huwa tunapitia katika upofu wa teknolojia mara kadhaa katika maisha yetu.


Aliyekuwa CEO wa kampuni ya Microsoft, Steve Ballmer. Mnamo mwaka 2007 ambapo iPhone ya kwanza ilizinduliwa alisema"iPhone haiwezi kupata nafasi yoyote muhimu katika soko la smartphones, haiwezi kuja tokea". Hakujua, alisema kauli hii kwa sababu ya kuwa na upofu wa teknolojia, iPhone ilikuwa ni simu ya kwanza kutumia teknolojia ya full capacitive touchscreen na smartphone karibuni zote zilizokuwepo muda huo kabla ya iPhone kuja zilikuwa zina physical qwerty keyboard, alisema kauli hiyo akiona kwamba hakuna mtu atayehitaji kutumia touchsreen smartphone. Angalia hali ilivyo sasa, kila mtu anataka touchscreen smartphone. Lakini ukirudi miaka saba nyuma watu wengi walikuwa na mashaka na kutumia simu hizi na kuona kwamba zitakuwa ngumu mno kutumia.


Huwa tunadhani ya kwamba teknolojia iliyopo katika muda fulani itabaki kuwa bora siku zote, na kuona teknolojia mpya itakuja kwa muda mfupi na kisha kuondoka zake. Tazama katika teknolojia ya smartwatches, kwa muda huu watu wengi wanaona ni kitu kisicho cha manufaa na pengine zitakuwepo kwa miaka sita au saba na kisha kupotea jumla. Lakini kadiri muda unavyozidi kwenda vifaa hivi vinazidi kuboreshwa, itafika mahali ambapo smartwatches zitachukua nafasi kubwa ya maisha yetu na tutasahau ya kwamba mwanzoni wakati vinaingia sokoni tuliona vinakosa maana kabisa. Mwaka 2011, dada yangu hakutaka kabisa kuitumia simu yangu kwa sababu ilikuwa ni touchscreen,aliniambia hivi" siwezi kutumia simu za touchscreen na sitaki hata kuzisikia", lakini leo hii, ninaonekana mshamba kwake katika matumizi ya full touchscreen smartphones!






No comments :

Post a Comment