Feb 15, 2014

Lenovo anajikita zaidi katika biashara ya smartphone!je, ataweza?

Lenovo, moja ya kampuni kubwa zinazotengeneza kompyuta duniani hivi karibuni ameinunua kampuni ya Motorola Mobility iliyokuwa ikimilikiwa na Google. Motorola imeuzwa kwa kiasi cha dola za kimarekani $2.91 bilioni, habari hizi za Lenovo kununua Motorola zimekuja siku moja kabla ya Google kutangaza mapato yake ya robo ya nne ya mwaka 2013(quarterly earnings). Ununuzi huu hautakuwa wa pesa taslimu jumla, Lenovo atatoa kiasi cha dola $660 milioni kama fedha taslimu, $750 zitakuwa hisa na kiasi kinachobaki kitalipwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

GOOGLE ALIPONUNUA MOTOROLA.
Google alinunua Motorola rasmi mnamo mwaka 2012 kwa kiasi cha dola za kimarekani 12.5$ bilioni, kwa upande wangu nilifurahishwa na hatua hii kwa sababu sikupenda kuona Motorola ikifa kutokana na ubora wa smartphone alizokuwa akitengeneza, ukikumbuka simu kama Motorola Defy Mini. Lakini hii ilikuwa ponea ya Motorola lakini ni janga kwa Google. Tangu aliponunua kampuni hii alizidi kupoteza fedha nyingi siku hadi siku, soko lina ushindani sana. Kuweza kupambana na kampuni kama Samsung au Apple si kitu kidogo kabisa, Google alijitahidi katika kipindi hiki chote lakini hakuweza kupata faida kama ile aliyotegemea.
MATEGEMEO YA LENOVO KWA MOTOROLA.
Kwa miaka mingi, Lenovo, ambayo ni kampuni ya China imejikita sana katika utengenezaji wa kompyuta hasa pale iliponunua biashara ya kompyuta za ThinkPad kutoka kwa IBM mnamo mwaka 2005. Hivi karibuni imeamua kuwekeza zaidi katika biashara ya kuuza smartphones, si kwao China tu bali dunia nzima. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hii Bwana Yang Yuanqing alisema kwamba “tunaamini wazi tutaweza badili  Motorola ambayo kwa sasa haileti faida kuwa kampuni yenye kuleta faida maradufu” aliongeza kwa kusema kwamba “katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kununua Motorola tunategemea kuuza smartphones takribani milioni 100 duniani kote”. Kipindi cha mwaka jana Lenovo ameuza takribani smartphones milioni 45, ongezeko la asilimia 90% ukilinganisha na mwaka 2012.
GOOGLE ANA LIPI LA KUSEMA?
Google anaonekana kuwa na matumaini makubwa kwa Motorola, si kwamba hatohusika kabisa. Uhusiano utaendelea kwa sababu bado ana hisa katika kampuni hii. CEO na mmoja wa wamiliki wa Google, Bwana Larry Page alisema “Ununuzi huu utasaidia kusukuma mawazo na nguvu zetu katika ubunifu na kuzidi kuboresha Android OS na kuleta faida kwa watumiaji  wake wote”. Google wanaamini Motorola anaweza kuwa moja ya vinara katika Android OS kama walivyo Samsung na HTC, pamoja itachukua muda kidogo.
Aliyekuwa CEO wa Motorola Mobility sasa amehamia Dropbox na huko atakuwa kama COO(Chief Operating Officer). Lenovo ana hamu kubwa sana ya kuteka soko hasa la Marekani, alionyesha nia kubwa sana katika kununua BlackBerry hapo mwaka jana. Lakini hakufanikiwa, hakukata tamaa na hatimaye kaweza kuchukua Motorola na hii itamsogeza karibu zaidi na soko la Marekani ambalo kiukweli, linaleta faida sana. Pia atajitangaza kidunia hasa katika masoko yanayochipukia(emerging markets) kama Africa, Asia na Latin Amerika.

No comments :

Post a Comment