Feb 25, 2014

Kwanini Facebook ameinunua Whatsapp?

Kwa kiasi kikubwa hili ni swali ambalo watu wengi sana wanajiuliza. Na majibu ya swali hili yapo mengi, mbali na watu kujiuliza kwanini Mark Zuckerberg ambaye ni mmiliki wa Facebook kaamua kununua app hii lakini pia watu wengi wanashangaa, ndo anunue kwa kiasi chote hicho!


Whatsapp imenunuliwa na Facebook kwa kiasi cha dola za kimarekani 19 bilioni(takribani trilioni 30 za Kitanzania). Ni kiasi kikubwa sana kwa kununua application, tena ya simu. Mwaka juzi Google alinunua kampuni ya Motorola kwa kiasi cha dola za kimarekani 12bilioni(takribani trilioni 19 za Kitanzania). Unaweza kuona ni jinsi gani Facebook wametumia kiasi kikubwa katika ununuzi huu. Viber hivi karibuni imenunuliwa na Rakuten kwa kiasi cha dola za kimarekani 900 milioni(sawa na trilioni 1.5 za Kitanzania) na ikiwa na watumiaji takribani milioni 300.

Facebook wanaonesha nia kubwa katika kujikita kwenye app mbadala ya SMS, ndo maana wameamua kununua Whatsapp. Whatsapp ina watumiaji takribani milioni 450, si nchi zote inafahamika sana. Nchi kama Japan, China na Korea haina umaarufu sana, apps kama WeChat, Line na Kakao Talk ndizo zinatumika sana katika nchi hizi. Pamoja na hilo sehemu nyingi za dunia zilizobaki ina watumiaji wengi sana. Whatsapp inatumika sana kama mbadala wa SMS sehemu hasa za Ulaya, Afrika, India, Latin Amerika na sehemu nyingine za Asia kama nchi za Uarabuni.

MPANGO WA FACEBOOK WA KULETA INTERNET KWA KILA MTU DUNIANI.

Facebook ana kampeni ya kuwezesha upatikanaji wa internet kwa kila mtu duniani, hasa katika nchi zinazoendelea. Kampeni hii inaitwa internet.org akishirikiana na makampuni mengine makubwa ya teknolojia kama Samsung, Qualcomm, Nokia na mengineyo. Ukiangalia nchi nyingi zinazoendelea mfano za Afrika na Asia zina watumiaji wengi wa Whatsapp lakini upatikanaji wa huduma ya internet si wa uhakika. Ina maana kama Facebok anataka boresha huduma ya internet katika sehemu hizi inambidi awe karibu na njia wanayotumia watu wa sehemu hizi katika mawasiliano ya internet, ambayo kwa kiasi kikubwa ni Whatsapp. Hapo mbeleni Whatsapp itamuwezesha mtumiaji kuweza kupiga simu kupitia njia ya internet, hii italeta urahisi maradufu kwa watu kuwasiliana. Ina maana watumiaji watazidi kuongezeka. Na kampeni ya internet.org ikifanikiwa kwa pamoja hivi vitu viwili vitaweza kuinua matumizi ya huduma ya internet kwa nchi zinazoendelea na kumfanya Facebook kufaidika pia. Mark Zuckerberg alisema "kama ukizileta Facebook na Whatsapp pamoja, itasaidia kuunganisha dunia kimawasiliano kwa urahisi na itasaidia kufanikisha kampeni kama ya internet.org". Mwaka 2012 Facebook alinunua app ya Instagram kwa kiasi cha dola za Kimarekani 1bilioni(trilioni 1.6 za Kitanzania). Instagram inafanya vizuri lakini si njia ya mawasiliano ukifananisha na Whatsapp, pamoja na Facebook kuwa na Messenger yao lakini watu wengi hawapendelei kiutumia, Whatsapp ina watumaji wengi kwa sababu ni rahisi sana kuitumia.

UWEPO WA MATANGAZO KATIKA WHATSAPP.

Whatsapp Messenger iko tofauti sana na apps nyingine, huwa hawaonyeshi matangazo(selling advertisements). Kwa upande mwingine, kinachompa faida Facebook ni matangazo hasa. Watu wengi wana wasiwasi pengine kuna uwezekano wakaanza kutangaza pia katika Whatsapp. Aliyekuwa mmiliki wa Whatsapp, Bwana Jan Koum alisema ya kwamba hakutakuwa na matangazo yoyote katika kutumia Whatsapp. Lakini kauli hii itakuwa kweli siku hizi za mwanzo, lakini hapo mbeleni ikifika watumiaji bilioni moja au mbili, hayo ni mazingira mazuri sana ya kutengeneza hela kutokana na matangazo.



No comments :

Post a Comment