Feb 3, 2014

Hahaha!kweli Nokia mnatapatapa?

Tangu mwaka jana kumekuwa na tetesi huku na kule katika mtandao zikielezea simu ya Nokia itayotumia Android Operating System, wengine wanasema itapewa jina la Nokia Normandy na wengine pia wanasema itaitwa Nokia X. Hakuna mwenye uhakika mpaka sasa kwa sababu simu hiyo haijazinduliwa rasmi.

Kiukweli, Nokia anahangaika. Mradi huu wa simu ya Android ulikuwepo tangu mwaka 2010 lakini aliupiga chini baada ya Microsoft kumuonyesha Windows Phone OS mwaka 2011,haya! kaenda nayo hiyo Windows Phone OS katika simu zake za Nokia Lumia lakini anaona kama haimilipi kisawasawa hivi.


Akaamua kufufua tena mpango wa kutengeneza simu ya Android, lakini baada ya taarifa tu kuzagaa mtandaoni kwamba Nokia ameamua kufanyia kazi mpango huo,wakakana taarifa hizo.Cha ajabu!kadiri siku zinavyokwenda picha zinazidi kuonekana mtandaoni zikionesha muonekano wa simu hiyo utavyokuwa. Wanafanya mambo kwa usiri mkubwa. Yote ya nini? Inaeleweka wazi kampuni hii tangu mwaka 2008 imekuwa haina misimamo imara, yote kwa sababu Android na iPhone waliibuka katika fani mida hiyo. Aliwahi kuja na Operating System inayoitwa Nokia Meego OS ikiwa katika Nokia N9 akaja ipiga chini, lakini software hiyo iliendelezwa na wafanyakazi wa zamani wa kampuni hiyo na ndiyo leo imetokea Sailfish OS ikitumika katika Jolla Phone, na inafanya vizuri mno hasa barani Ulaya.
Muonekano wa Nokia Normandy au Nokia X.

Simu hii inaonekana inatumia Android lakini muonekano wake bado una mfanano mkubwa na Windows Phone. Swali,Nokia unataka kuwakoroga vichwa wateja wako? wapate ugumu kutofautisha ni Nokia ipi inatumia Android na ipi inatumia Windows Phone OS! Bado sijaelewa lengo lao ni lipi hasa. Tusubiri tuone hiyo simu ikitoka rasmi, pengine itakuwa cha kitu mojawapo cha tofauti na hakijawahi tokea katika smartphone yoyote ile.

Si kwamba sizipendi Nokia,la hasha. Ni mpenzi mkubwa tu na hata smartphone yangu ya kwanza ilikuwa ni Nokia. Wanachotakiwa ni kuwa makini na maamuzi yao, hasa mida kama hii yenye changamoto kibao katika soko. Apple kila siku anazidi kuwa mbunifu,Samsung,HTC,LG na wengine wengine wanaonyesha cheche zao. Kazi kwake Nokia!

No comments :

Post a Comment