Nov 22, 2013

Huenda ikazaliwa Silicon Valley nyingine nchini Finland,hili linachangiwa na kuanguka kwa Nokia.

Silicon Valley ni sehemu iliyopo jimbo la California nchini Marekani,hapa ndipo nyumbani kwa makampuni mengi makubwa ya teknolojia duniani.Apple,Google,Yahoo,Adobe Systems na kadhalika.Si tu kwamba yanapatikana makampuni makubwa bali hata yale yanayochipukia mengi yao yanapiga makazi hapa.Unaweza fikiria ni jinsi gani sehemu hii ilivyokaa kiteknolojia zaidi,watu wa eneo hilo maongezi yao mengi yanatawaliwa na teknolojia.

Nchi ya Finland ni mojawapo ya nchi zilizopo barani Ulaya zenye namba ndogo sana ya watu,ina asilimia kubwa sana ya watu walioelimika.Nchi hii ina takribani watu milioni tano na nusu,kwa hapa kwetu ni sawa na kuchukua idadi ya watu waliopo Dar-Es-Salaam tu.

Nchii hii inaanza kuwa kivutio kikubwa cha wanateknolojia na wawekezaji katika sekta hii.Miaka mitano iliyopita mkurugenzi wa masoko wa kampuni ya Rovio(watengenezaji wa game la Angry Birds) alianzisha mkutano unaoitwa kwa jina la Slush,ni mahususi kwa wanateknolojia hasa wa barani Ulaya kukutana na kujadili kuhusu changamoto za teknolojia na pia ugunduzi gani uliofanyika toka mkutano uliopita.

Mkutano huu hufanyika katika moja ya kiwanda kilichokuwa kinatumika na kampuni ya Nokia kati ya miaka ya 1990 hadi 2000 katika tafiti zake.Tangu kuanzishwa kwa mkutano huu,umeonesha kuzidi kuvuta wengi mwaka hadi mwaka.


Tukirudi nyuma miaka kama kumi iliyopita enzi hizo Nokia akishika soko kwelikweli.Nchini Finland ilikuwa hivi,ukimuuliza mtoto mdogo akikua atataka kufanya kazi kampuni gani? basi jibu lilikuwa ni "Nokia".Kadiri miaka ilivyozidi sogea hali ikaanza kubadilika na kuwa mbaya kwa kampuni hii.Hii ni baada ya makampuni kama Google na Apple kuanza kujikita zaidi katika kutengeneza smartphone.

 Nokia akaanza kupunguza wafanyakazi na pia kufunga baadhi ya viwanda vyake baada ya kuanza kupoteza masoko ya bidhaa zake.

 Watu waliopunguzwa na pia wawekezaji waliamua kuchukua hisa zao toka Nokia na ndiyo leo wanaanzisha makampuni ya teknolojia ambayo mengi yanapata mafanikio.Kampuni kama Rovio na Supercell(wanatengeneza game la Clash Of Clans na Hayday) yanazidi kupata utambuzi mkubwa hasa katika katika OS za Android na iOS.

Hii inaonyesha wazi kwamba Finland inaweza kung'aa bila Nokia.Ni bora kuwa na makampuni mengi yanayofanya vizuri kuliko na nchi kuwa na utegemezi wa kampuni moja tu.

Wakazi wa Finland ni watu wenye aibu sana na uoga.Lakini kwa sasa,hali hii inaanza kuwatoka pale wanapoona mtu mmoja anaanzisha kampuni ndogo tu na baada ya muda mfupi anapata mafanikio,hii inapelekea na wengine kujiuliza "kwanini na mimi nisifanye kama yeye?".Wengi wanaanza bila aibu wala uoga kwa hamasa hiyo.








Kwa nchi kama hii,mtu mmoja anapopata mafanikio basi ni mafanikio kwa nchi nzima.Kuja kwa mafanikio poa kunachangiwa sana na msaada wa serikali katika ku-support sekta binafsi zilizopp nchini humo.Si hivyo tu,watu hawa wanapenda kuchapa kazi pia.Kampuni ya Rovio imefanikiwa na game la Angry Birds lakini hapo nyuma alitengeneza games karibia 52 lakini hamna hata mmoja iliyofanikiwa.Hii inaonyesha ni jinsi walianzia mbali lakini pamoja na kufeli kote huko lakini hawakukata tamaa.

No comments :

Post a Comment