Teknolojia inazidi kukua siku hadi siku, na kwa kasi ya ajabu sana. Kama wanadamu, tunatakiwa tambua ya kwamba " unapotumia sana mawasiliano ya internet na ndivyo unajitenga na mawasiliano ya kidunia(physical interactions)". Teknolojia inatuondoa katika mazingira yanayotuzunguka na kutupeleka katika mazingira ambayo si halisi, tuna marafiki wengi wa mitandaoni kuliko marafiki tulionao shule au kazini. Tunatumia muda mwingi katika smartphones zetu kuliko kuongea na wale wanaotuzunguka.
Miaka ya zamani, kabla ya teknolojia kuitawala dunia watu walikuwa wakienda sehemu wasizozijua kwa kuelekezwa na mtu mwingine au kutumia ramani iliyopo katika karatasi. Tofauti na siku hizi, hatujui hata kusoma ramani, tunapata shida kujua alama za barabarani na hatuna muda wa kusoma maelezo yaliyopo njiani na katika majengo. Unaenda sehemu usiyofahamu? Sawa! Google Maps itakuelekeza kuanzia ulipo na upite wapi mpaka kufika unapohitaji kwenda, rahisi sana eeh!