Miaka ya nyuma, Samsung amelalamikiwa sana kuhusu matumizi ya plastiki na ubunifu (design) hafifu wa smartphone zake. Yote yamepita na sasa imebaki historia, Kiswahili kizuri tunasema "ya kale". Ninasema " ya kale" kwa sababu sasa hivi Wakorea Kusini hawa wametambua ubunifu bora na unaokwenda na wakati, hili linajidhihirisha katika flagship smartphones zao za sasa, Samsung Galaxy S6 na Galaxy S6 Edge ambazo muundo wake wa nje umetengenezwa kwa kutumia metali ya Aluminum na Kioo kigumu (tempered glass) kinachozuia michubuko(scratch resistant) kinachofahamika kama Gorilla Glass 4. High-Tech Computer Corporation, wanafahamika maarufu zaidi kama HTC wanajua ubunifu bora wa smartphones, sio siri! Na hata wakati Samsung analalamikiwa kwa kutumia plastiki katika Samsung Galaxy S4 mnamo mwaka 2013, HTC alifahamu vizuri zaidi jinsi ya kutumia Aluminum na sio plastiki katika kutengeneza umbo la nje la HTC One M7, iliyokuwa mpinzani (rival) wa Galaxy S4.
Japokuwa HTC anafahamu vizuri ubunifu wa simu na ndiye wa kwanza kutumia metali kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa smartphone zake, suala la kushindwa kuwa na kamera nzuri katika smartphone hizo linamnyima usingizi kabisa. Si kwamba kamera ya HTC One M8 (flagship yao ya 2014) ni mbaya, lakini ina ubora gani ukiifananisha na kamera ya smartphone kama LG G3 au Sony Xperia Z3 kwa mfano, ambao wote hawa ni wapinzani wake (rival smartphones).